PATA MATUKIO MBALI MBALI YA KIJAMII POPOTE ULIPO!

Thursday, September 30, 2010

Pombe Pombe: Je, tutafika?

Tuepuke Pombe kwani ni hatari kwa maisha yetu. 

Inaelekea ni vigumu sana wale waliozoea pombe kukubali ukweli kwamba unywaji wa pombe unaongeza uwezekano wa kupata saratani na magonjwa mengine.  Ukweli ni kwamba pombe inaongeza sana uwezekano wa kupata saratani hasa zile za koo, kinywa  ini na matiti.  Pamoja na matatizo hayo ya kiafya, pombe inaingilia uwezekano wa kufanya maamuzi mazuri, ikiwa ni pamoja na wakati wa kuendesha gari.  Kwa maana hiyo pombe huchangia sana ajali za barabarani.  Na kwa kuwa ajali za barabarani zinasababisha vifo na kufupisha maisha, ninaamini pombe ni kitu cha kuepuka sana.  Ndio maana hata polisi wa usalama barabarani wanamchukulia hatua mtu ambaye amekunywa pombe na kuendesha gari, na pia wakati mwingine wanazo mashine maalum za kumpima mtu ili kugundua kama amekunywa pombe kiasi kinachoathiri maamuzi.
Epuka matumizi ya pombe

Cha ajabu ni kwamba katika  wiki ya usalama barabarani hapa kwetu Tanzania (Dar es Salaam) 2010, kampuni moja ya bia imetoa msaada kwa polisi (kikosi cha usalama Barabarani), na msaada huo ni pamoja na stika zinazotangaza usalama barabarani lakini hapo hapo zinatangaza pombe.  Polisi hao kwa mikono yao wenyewe wameonekana wakibandika stika hizo zinazotangaza pombe kwenye magari. http://issamichuzi.blogspot.com/2010/08/tbl-yatoa-vifaa-vyenye-thamani-ya-zaidi.html Nadhani hapa kuna mgongano wa nia au taratibu ( “conflict of interest”).  Inasemekana kwamba kampuni hiyo imetoa pia fulana zenye ujumbe wa usalama barabarani lakini naamini pia zinatangaza pombe.  Naamini kikosi cha usalama barabarani wanahitaji kufikiria tena uamuzi wao huo wa kufadhiliwa na kampuni inayotengeneza pombe huku wakitangaza pombe. Iwapo imebidi kupokea ufadhili huo basi ni muhimu kikosi hicho kukubaliana na kampuni hiyo kwamba ufadhili huo hautahusisha matangazo ya pombe wala ya kampuni yao.
Naamini wengi wetu tungependa kutangaza usalama barabarani bila kutangaza pombe!  Tunapenda kutangaza vitu vinavyoongeza ubora wa maisha sio vinavyopunguza ubora wa maisha. Tukumbuke kwamba pombe pamoja na kuchangia ajali za barabarani, inachangia sana kuongeza uwezekano wa kupata saratani hasa zile za koo, kinywa, ini na matiti. http://jipende.com/archives/tag/alcohol/ .
Tuepuke matumizi ya pombe.  Jipende, ufunguo wa mtindo bora wa maisha upo mkononi mwako!
Epuka matumizi ya pombe
 

Habari hii ni kwa msaada wa mtandao wa Aunt ;Mary G. Materu, (Msc)

unaweza kutembelea Jipende.com

No comments:

Post a Comment