PATA MATUKIO MBALI MBALI YA KIJAMII POPOTE ULIPO!

Saturday, October 9, 2010

POLENI TAIFA STARS!! TUKAZE BUTI SAFARI NDEFU..

wachezaji wa Taifa Stars wakiingia uwanjani wakiongozwa na kipa Juma Kaseja

kikosi cha Taifa stars hii leo  kabla ya mechi



Timu yetu ya Taifa Stars leo imefungwa bao 1-0 na Moroco
TIMU ya soka ya Tanzania  ‘Taifa Stars,’  leo  ilishindwa kuutumia uwanja wake wa nyumbani baada ya kuchapwa bao 1-0  na Morocco katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Jakaya Kikwete.

Ikitoka kuvuna sare ya bao 1-1 dhidi ya Algeria katika mechi ya kwanza ya kundi D iliyochezwa Septemba 3, mjini Algiers, Stars leo  ilishindwa kuonyesha kiwango kizuri.


Kipigo hicho kimeiweka Stars katika wakati mgumu kwenye kampeni ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika zitakazochezwa nchini Gabon na Guinea ya Ikweta mwaka 2012.
Wakati Morocco ikifikisha pointi nne baada ya kuvuna sare ya bila kufungana na Afrika ya Kati katika mechi ya Septemba 4, Stars imebaki na pointi moja huku Algeria na Afrika ya Kati zikicheza leo.
Katika mechi ya jana, Stars iliyo chini ya Kocha Jan Poulsen, ndiyo ilianza kwa kasi huku Morocco wakionekana kutumia muda mwingi kuusoma mchezo.


Stars walitawala mchezo huo katika dakika 20 za mwanzo kwa viungo wake kumudu kupasiana, lakini kazi kubwa ilikuwa ni kuipenya ngome ya Morocco.

Kwa mfumo huo, licha ya Stars kuonekana kuwa na mpira mara nyingi huku Moroco wakicheza mpira mwepesi, bado ilikuwa kazi kubwa kumfikia kipa wa Morocco.

Nafasi mojawapo kwa upande wa Morocco, ilikuwa ni dakika ya tisa pale Marouane Chamakh, nyota anayechezea klabu ya Arsenal ya England, alipopata mpira lakini tayari alikuwa ameotea.

Moroco walionekana kucheza mfumo wa kujilinda zaidi na kufanya mashambulizi machache tofauti na washambuliaji wa Stars ambao walionekana kukosa mbinu za kuupenya ukuta wa wapinzani wao.

Ikiwachezesha Mrisho Ngassa na Danny Mrwanda pekee kwa safu ya mbele, walionekana kushindwa kukabiliana na mabeki wa Moroco kiasi cha kuwafanya wacheze watakavyo.

Dakika ya 42, Morocco walifanya shambulizi na kupata bao likifungwa na El Hamdoui Mounir anayechezea klabu ya Ajax ya Uholanzi, akiitumia vizuri pasi ya kichwa kutoka kwa Chamakh.
Hadi mwamuzi Sochurn Raji kutoka Mauritius anamaliza dakikia 45, Morocco walikuwa mbele kwa bao hilo moja, lakini kabla ya filimbi hiyo, Stars ilipata kona tatu mfululizo.

Kipindi cha pili, Moroco walirejea uwanjani kwa staili tofauti ambayo walicheza kwa kutoa pasi za haraka, hali ambayo iliwachanganya zaidi Stars.
Morocco waliendelea kulinda lango huku wakishambulia, hali ambayo ilizidi kuwapoteza Stars ambao walishindwa kuepuka kipigo mbele ya Rais Kikwete.

Akizungumzia matokeo hayo, Kocha wa Stars Jan Poulsen alisema Moroco ni timu bora kwani waliweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga huku akisifu pia safu ya ulinzi ya wapinzani wao.
Alisema kutokana na kutokea faulo nyingi, alimkumbuka kiungo wa timu hiyo, Abdi Kassim, kwa umahiri wake wa kupiga mipira ya adhabu.
Alisema kama Babi angekuwepo katika mechi ya jana, Stars ingeweza kupata bao kama alivyofanya katika mechi ya Septemba 3 dhidi ya Algeria.
Kuhusu wachezaji wake kucheza chini ya kiwango, alisema hiyo hutokea kama ilivyo kwa Chamakh ambaye jana alicheza kama hayupo uwanjani.
Naye Kocha wa Moroco, Dominique Cuperly, alisema licha ya vijana wake kushinda, Stars ni timu nzuri kwani wachezaji wake walicheza kwa ari kubwa.

Stars: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Stefano Mwasyika, Aggrey Morris, Nadir Haroub Cannvaro, Henry Joseph/Mohamed Banka, Idrssa Rajab/Salum Machaku, Nizar Khalfan/John Bocco, Shaban Nditi, Mrisho Ngassa na Danny Mrwanda.

Morocco: Lamyaghri Nadir, Kharja Houssine, Basser Michael, El Moutaqui Mehdia, Kantari Ahmed, Soulaiman Rachid, Hermach Adil, Elahmad Aroussi Karim/Berrabeh Mohamed, Boussoufa Mbarek, Chamakh Marouane/ El Arabi Youssef, El Hamdoui Mounir/Hadji Youssouf.

No comments:

Post a Comment