Baadhi ya watoto wa Chipukizi (CCM) wilaya ya Kinondoni wakiimba wimbo wa kudai haki za watoto hivi karibuni
Dar es Salaam; Haki mtoto Blog Team
WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kuripoti mambo mazuri yanayofanywa na watoto badala ya kuandika mabaya pekee yanayofanywa na watoto hao.
Changamoto hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Ofisa Uchunguzi Mkuu wa masuala ya Haki za Binadamu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, Alloyce Komba, wakati wa warsha kwa waandishi wa habari kuhusu wajibu wao katika kuripoti habari za watoto.
“Walindeni watoto mnapofanya kazi zenu kwani nao wana haki kama wengine, ikiwemo ya kuwa na faragha, kulindwa na kufanyiwa mambo mema, msiishie kuripoti matatizo yao tu,” alisema Komba ambaye pia ni Mwanasheria wa Tume ya haki za binadamu.
Naye Mwenyekiti wa Mashirika yanayounda Ajenda ya Watoto, Euster Mwaituka, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Afya, Maendeleo na Kutetea Haki za Watoto na Wanawake (KIWOHEDE) alisema kwa sasa bado ukiukwaji wa haki za watoto unaendelea kufanyika.
Warsha hiyo ya siku tatu imeandaliwa na Mtandao wa Mashirika ya Ajenda ya Watoto na kuratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Ukimwi (AJAAT) kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
No comments:
Post a Comment