RAIS Jakaya Kikwete, ameendelea kumwaga ahadi zake kwa wapiga kura ambapo jana amewaahidi wafugaji nchini kuwa atawatengea maeneo maalumu kwa ajili ya malisho ya mifugo yao .
Ahadi hiyo aliitoa mapema keo katika Jimbo la Mikumi lililopo mkoani Morogoro, alipokuwa akiendelea na kampeni za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa rais kwa kipindi kingine cha miaka mitato sambamba na kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo hilo , Abdisalaam Ameir.
Kikwete, alisema lengo la kuwatengea maeneo wafugaji ni kuwaepusha na migogoro inayotokea mara kwa mara kati yao na wakulima.
Katika mkutano huo, Kikwete aliwaomba wakazi wa Mikumi kuichagua CCM, ambayo imedhamiria kukomesha mivutano ya wafugaji na wakulima.
“Maisha ya kuhamahama ya wafugaji ifike mahala tusema basi… lazima maisha hayo yawe na mwisho, tumejipanga kutenga maeneo maalumu ya kufugia, tumedhamiria kuweka sehemu maalumu za malisho ya mifugo yenu kwenye maeneo mengi kadiri iwezekanavyo.
“ Katika kipindi cha miaka mitano kazi hiyo itakamilika na wafugaji wataona fahari,” alisema.
Kikwete, alisema anaridhishwa na kasi ya uandikishaji wa watoto kwa shule za msingi ambapo Wilaya ya Kilosa imefanikiwa kwa kiwango cha asilimia 93 ya uandikishaji.
Kuhusu miumdombinu ya barabara, mgombea huyo alisema sh bilioni 1.7 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa barabara za vijijini wilayani humo na kuongeza kwamba kasi zaidi itakuwepo kwa miaka mitano ijayo ili kuhakikisha kero ya usafiri inafika ukomo.
Alisema anahuzunishwa na kasi na kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), ambapo kwa Wilaya ya Kilosa jumla ya wagonjwa 2,329 wanapatiwa dawa za kupunguza makali ya virusi huku akibainisha kuwa kwa Mkoa wa Morogoro wagonjwa 24,338 wanapatiwa huduma hiyo.
Alisema kiwango hicho cha wagonjwa ni kikubwa mno ambapo maambukizi kwa Kilosa peke yake ni sawa na wastani wa asilimia 3.8 wakati wastani wa taifa ni asilimia 5.8.
Kwa mujibu wa malaria, alisema serikali imefanikisha utoaji wa vyandarua 113,848 vilivyosambazwa mkoani hapa huku akiwataka wananchi waliokosa vyandarua kuwaeleza viongozi wa kata na vijiji walio karibu nao.
No comments:
Post a Comment