PATA MATUKIO MBALI MBALI YA KIJAMII POPOTE ULIPO!

Friday, October 15, 2010

LHRC KUTOA MATOKEO KILA JIMBO!

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, kinatarajia kutoa matokeo ya wagombea kwa kila jimbo kwenye mtandao katika kipindi cha uchaguzi.
Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa kituo hicho, Ezekiel Masanja, alibainisha hayo mapema leo jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa mafunzo ya siku mbili kwa waangalizi wa ndani wa uchaguzi kutoka mashirika mbalimbali.
       
Alisema mbali na kutoa matokeo kupitia tovuti yao ya www.uchaguzi.or.tz pia wananchi nao watapata fursa ya kutuma taarifa mbalimbali ya hali inavyoendelea katika vituo mbalimbali vya kupigia kura.
Alisema,  lengo la waangalizi hao si kuingilia kazi ya Tume ya Uchaguzi (NEC) bali ni kuhakikisha uchaguzi unakwenda kwa haki.

Aidha, alisema wananchi wanaweza kutuma ujumbe kupitia namba 15540 kutoa taarifa ya tukio lolote litakalokwenda kinyume na taratibu za sheria na wao baada ya kulifuatilia na kulipatia uhakika wataliweka mtandaoni.

Kwa mujibu wa Masanja huduma hiyo itakuwa bure ambapo aliwataka wananchi kuwapa ushirikiano waangalizi hao ili kuufanya uchaguzi kuwa huru na wa haki.
Wakati huohuo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema wanaridhishwa na hali ya kampeni inavyoendelea, japokuwa yapo maeneo machache ambayo fujo zimejitokeza.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstahafu Lewis Makame, aliyataja maeneo hayo kuwa ni Musoma, Moshi na Arusha.

No comments:

Post a Comment