PATA MATUKIO MBALI MBALI YA KIJAMII POPOTE ULIPO!

Thursday, October 21, 2010

MTOTO AOKOTWA NDANI YA BASI

BUNDA, MARA


MTOTO mdogo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne, ameokotwa akiwa ametelekezwa ndani ya basi wilayani Bunda mkoani Mara.

Mtoto huyo wa kiume anayezungumza kwa tabu aliyejitambulisha kwa jina la Thomas Marko, alikuwa amevaa nguo ambazo ni suruali nyeusi na shati bluu iliyoandikwa namba 51 mgongoni.

Tukio hilo lililothibitishwa na Polisi wilayani Bunda, lilitokea mwanzoni mwa mwezi huu majira ya jioni, wakati basi hilo lijulikanalo kwa jina la Ellys Express, lilipokuwa likitokea jijini Mwanza likiekea wilayani Bunda.

Kwa mjibu wa wafanyakazi wa basi hiyo inayofanya safari zake kati ya Bunda na jijini Mwanza, mtoto huyo aligundulika kuwa ametelekezwa ndani ya basi hilo, baada ya kufika katika kituo cha Lamadi, wilayani Magu.

Imeelezwa kuwa baada ya kuuliza kila abiria aliyekuwa katika gari hilo hakuna abiria hata mmoja, aliyekubali kwamba mtoto huyo ni wake.

Aidha, wafanyakazi wa basi hilo wamesema kuwa baada ya kufika katika kituo cha mwisho ambacho ni cha Bunda mjini,  walimchukuwa mtoto huyo na kumpeleka polisi katika kituo kikuu cha Bunda.

Kwa sasa mtoto huyo anaishi nyumbani kwa mfanyakazi mmoja wa basi hilo aitwaye Baina Mgisha, katika barabara ya Bomani mjini Bunda, baada ya polisi kumkabidhi mbele ya balozi wa eneo hilo kwamba amtunze akisubili kutambliwa na wazazi wake.

'Hata hajui kuzungumza bali anatajajina lake na la baba yake tu, wala nyumbani kwao hapajui, tukimuuliza anasema ni mbali' alisema mwanamke mmoja anayeishi na mtoto huyo.

Mwandishi wa habari hizi baada ya kupata taarifa za kuhusu mtoto huyo, jana alifika nyumbani hapo na kumkuta akiwa na afya njema, lakini hajui kujieleza kutokana na umri wake kuwa mdogo kwani anajua kutaja jina lake na la baba yake tu, wala nyumbani kwao hapajui.

Yeyote aliyepotelewa mtoto wake awasilianane na mwandishi wa habari hizi kwa simu namba zifuatazo, ili amwelekeze mtoto wake alipo. 0784643040,0774643040,0655643040,0765647577

No comments:

Post a Comment